Video and Shared space ads

Thursday, August 2, 2012

Karibuni Washairi Kutoka Nyikani na Mijini

Wataka toa neno toka moyoni,
Wataka achia dukuduku toka rohoni,
Wataka dondosha andiko kibaoni,
Wataka achia chozi toka machoni,
Karibu ujiachie jamvini na andiko la ufukweni;

Utakapo penda kuona watu wakisoma shairizo,
Tafadhali usisite kunitumia beti hizo,
Nizipambe kurasani na vibwagizo,
Watu waweze zisoma ili na wewe uwe gumzo.

Kwenye barua pepe: info@jinlepoet.com
Nitumie jina lako kamili.
Ahsante.

Tuesday, April 10, 2012

KANUMBA THE GREAT (R.I.P)



Kama barafu juani umeyeyuka,
Kama mshumaa kwenye upepo umezimika,
Jumamosi alfajiri umetutoka,
Kanumba the great tutakukumbuka.

Nje ya mipaka ya nchi umetuwakilisha,
Nollywood mpaka Hollywood umefika,
Bendera ya Tanzania kuitangaza,
Kanumba the great tutakukumbuka.

Sunday, March 25, 2012

SIO LINGINE BALI KUTAKA KUKUTULIZA


Kwanza naanza kwa kutambaza,
Maneno matamu kukuliwaza,
Moyo wako kuusuuza,
Sio lingine bali kutaka kukutuliza;

Wengi wamekuliza,
Machoni wakakutuliza,
Moyoni wakakupoteza,
Fikirani mwao hukuingizwa,
Sina lingine bali kutaka kukutuliza;

Ahadi naiwekeza,
Kapuni naitupia,
Ubani ntajifukiza,
Marashi ntakunyunyiza,
Kwa pamoja tutanuiza,
Sio lingine bali kutaka kukutuliza;

Friday, March 23, 2012

CHA MWIKO UTAKIONA


Ukumbini najongea, Kwa kitambo nimemezea,
Mengi nimejionea, Baharini yalojitokezea,
Dunia imejichokea, Kwa binadamu ni mazoea,
Lamba lamba kama asali, cha mwiko utakiona;

Ujio huu sio wa ukali, bali kwa kile nlichokiona,
Uvumi umekuwa kauli, Kwamba sicho wanachokinena,
Wewe umsafi kiakili, mpaka kimwili unajivuna,
Lamba lamba kama asali, cha mwiko utakiona;

Thursday, March 22, 2012

SIKU YA MAJI DUNIANI



Maji yana rangi ya tope, na hayapatikani nchini kote,
Maji yamejazwa vyombo vyote, hamna hata cha kuwekea matoke,
Hawasemi lini watayaachia yatoke, japo nguo za ofisi zioshwe,
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

Wakina mama na watoto foleni bombani,Huku maneno wakirushiana hadharani,
Siku ya pili leo hawajaenda shuleni,Wanawasaidia wazazi kisimani,
Adha hii inajulikana serikalini, wakulitatua hatujui ni nani?
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

Wengine wanaoshea magari, wengine wamwagilia bustani,
Wengi hawana hata ya kutia kinywani, wengine hawajawahi tia bomba machoni,
Maji bidhaa adimu sio vijijini tu bali hata mijini, na hatujui yataisha lini?
Labda tutumie ya baharini kwa matumizi ya nyumbani,
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

 Imeandaliwa na Ally Bukuku/Buchicks