Video and Shared space ads

Thursday, August 2, 2012

Karibuni Washairi Kutoka Nyikani na Mijini

Wataka toa neno toka moyoni,
Wataka achia dukuduku toka rohoni,
Wataka dondosha andiko kibaoni,
Wataka achia chozi toka machoni,
Karibu ujiachie jamvini na andiko la ufukweni;

Utakapo penda kuona watu wakisoma shairizo,
Tafadhali usisite kunitumia beti hizo,
Nizipambe kurasani na vibwagizo,
Watu waweze zisoma ili na wewe uwe gumzo.

Kwenye barua pepe: info@jinlepoet.com
Nitumie jina lako kamili.
Ahsante.

Tuesday, April 10, 2012

KANUMBA THE GREAT (R.I.P)



Kama barafu juani umeyeyuka,
Kama mshumaa kwenye upepo umezimika,
Jumamosi alfajiri umetutoka,
Kanumba the great tutakukumbuka.

Nje ya mipaka ya nchi umetuwakilisha,
Nollywood mpaka Hollywood umefika,
Bendera ya Tanzania kuitangaza,
Kanumba the great tutakukumbuka.

Sunday, March 25, 2012

SIO LINGINE BALI KUTAKA KUKUTULIZA


Kwanza naanza kwa kutambaza,
Maneno matamu kukuliwaza,
Moyo wako kuusuuza,
Sio lingine bali kutaka kukutuliza;

Wengi wamekuliza,
Machoni wakakutuliza,
Moyoni wakakupoteza,
Fikirani mwao hukuingizwa,
Sina lingine bali kutaka kukutuliza;

Ahadi naiwekeza,
Kapuni naitupia,
Ubani ntajifukiza,
Marashi ntakunyunyiza,
Kwa pamoja tutanuiza,
Sio lingine bali kutaka kukutuliza;

Friday, March 23, 2012

CHA MWIKO UTAKIONA


Ukumbini najongea, Kwa kitambo nimemezea,
Mengi nimejionea, Baharini yalojitokezea,
Dunia imejichokea, Kwa binadamu ni mazoea,
Lamba lamba kama asali, cha mwiko utakiona;

Ujio huu sio wa ukali, bali kwa kile nlichokiona,
Uvumi umekuwa kauli, Kwamba sicho wanachokinena,
Wewe umsafi kiakili, mpaka kimwili unajivuna,
Lamba lamba kama asali, cha mwiko utakiona;

Thursday, March 22, 2012

SIKU YA MAJI DUNIANI



Maji yana rangi ya tope, na hayapatikani nchini kote,
Maji yamejazwa vyombo vyote, hamna hata cha kuwekea matoke,
Hawasemi lini watayaachia yatoke, japo nguo za ofisi zioshwe,
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

Wakina mama na watoto foleni bombani,Huku maneno wakirushiana hadharani,
Siku ya pili leo hawajaenda shuleni,Wanawasaidia wazazi kisimani,
Adha hii inajulikana serikalini, wakulitatua hatujui ni nani?
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

Wengine wanaoshea magari, wengine wamwagilia bustani,
Wengi hawana hata ya kutia kinywani, wengine hawajawahi tia bomba machoni,
Maji bidhaa adimu sio vijijini tu bali hata mijini, na hatujui yataisha lini?
Labda tutumie ya baharini kwa matumizi ya nyumbani,
Leo ni siku ya maji duniani, tuikemee au tuisherehekee?

 Imeandaliwa na Ally Bukuku/Buchicks


Wednesday, March 21, 2012

NYAMA CHOMA



Harufu ya ndimu na kitunguu swaumu, imetawala kiwanjani,
Majiko na kuni ngumu, moshi wapaa angani,
Naongelea nyama nyekundu, iliyowekwa jikoni,
Tumefuata nyama choma, au kuona nyama nona??

Tangawizi na pilipili manga, hazikukosa mezani,
Hususan kwa nyama nyeupe, kuku, bata au samaki,
Jasho zawamwagika, naongelea wapishi jikoni,
Tumefuata nyama choma, au kuona nyama nona??

Kiingilio buku tano, mlangoni kulipishwa,
Humo ndani ni michorano, na mavazi kuonyeshwa,
Ni kama kwenye mikutano, meza zimevyopangwa,
Tumefuata nyama choma, au kuona nyama nona??

Vimini na pedo pusha, vimetawala humo ndani,
Mabinti wamependeza, waonyesha hadi nguo za ndani,
Wakaka mate yawatoka, wakimsaka wakumuweka ndani,
Tumefuata nyama choma, au kuona nyama nona??

Mwakani itakuja tena, naomba niwahabarishe,
Msikose kuja tena, ili siku tuiboreshe,
Kwaheri ya kuonana, ngoja niwapishe,
Tumefuata nyama choma, au kuona nyama nona??

 Imeandaliwa na Ally Bukuku/Buchicks




Thursday, March 15, 2012

MADILI BILA MAADILI


Kukuru kukuru batini, kila ifikapo alfajiri,
Yowe nyumba ya jirani, mchawi kaingia ndani,
Majirani hawaamini, kwani hakusikia muadhini?
Madili bila maadili, haingii akilini.

Watoto yatima mitaani, msaada akilini,
Aliyepewa amali, miguu kanyoosha kibarazani,
Pesa kaweka kibindoni, mbwembwe nyingi mtaani,
Madili bila maadili, haingii akilini.

Kaomba kura ili kula, au kura kuwajibika,
Wananchi wamekunja sura, machozi kuwabubujika,
Waliomchagua wabadili taswira, uchaguzi ujao atawakumbuka,
Madili bila maadili, haingii akilini.

Wazazi wao wamewatoka, mlezi kaibuka,
Watoto wadogo yatima, mali zao kazichota,
Maisha duni wanapata, yeye wa kwake wajitamba,
Madili bila maadili, haingii akilini.

Vijana kifungoni, wameishakuwa mateka,
Wakiume wapelekwa vitani, wakike kimapenzi watumika,
Hii ni jamii yakina Joseph Kony, eti haki watafuta,
Madili bila maadili, haingii akilini.

Imeandaliwa na Ally Bukuku/Buchicks